SERIKALI KUJENGA ZAHANATI KIJIJI CHA KILEMBA
Posted on: May 7th, 2024Mwenyekiti wa kijiji wa Kilemba kata ya Mkigo halmashauri ya wilaya ya Kigoma Issa Kihamuzi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa shilingi milioni 100 kwaajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji chao.
Amesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kuondoa changamoto ya wananchi kutibiwa katika zahanati ya Mkigo, hospitali ya Heri Miission na Nyamasovu iliyopo halmashauri ya wilaya ya Buhigwe pamoja na kituo cha afya cha Matyazo.
“Wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya, kutoka Kilemba mpaka Mkigo wananchi hutembea kati ya nusu saa hadi saa moja na nusu, na inapotokea dharura ya magonjwa ya usiku au wajawazito inatubidi kukodisha gari kwa gharama kubwa kuanzia elfu 30,000-50,000”. Amesema Kihamuzi
Mwenyekiti ameongeza kuwa changamoto zaidi ipo kwa akina mama wajawazito ambao inawabidi kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika zahanati ya kata ya Mkigo ambapo baadhi yao hupatwa na changamoto ya kupoteza watoto au wao wenyewe kupoteza maisha na hivyo kukamilika kwa zahanati hiyo kutaokoa maisha ya mama na mtoto.
Hata hivyo Mwenyekiti amesema kukamilika kwa zahanati hiyo ya kutarahisisha huduma za afya kwa wananchi wa kata za jirani na nchi jirani ya Burundi, vilevile itasaidia kupunguza gharama za usafiri ambazo wananchi wamekuwa wakizipata.
Mwenyekiti Kihamuzi amemuomba Rais mara zahanati hiyo itakapokamilika wapelekewe vifaa vyote muhimu pamoja na wafanyakazi ili kuboresha huduma hizo.
Naye Eliasia Mayani mhudumu wa wa afya ngazi ya jamii, amefurahishwa na hatua ya serikali ya kuwajengea zahanati kwakuwa watapungunguza changamoto ya ushawishi kwa kina mama wajawazito kuanza huduma za kliniki mapema i kwakuwa watapata kwa kijiji mwao pa bila kutembea umbali mrefu.
Naye Nyamang’elele Mtaki afisa mifugo kata ya Mkigo, amesema hakukuwa na utulivu wa wafanyakazi kutokana na kukosekana kwa huduma za afya, anaamini zahanati hiyo itakapokamilika itakuwa chachu kwa watumishi kutulia katika vituo vyao vya kazi.