TUCTA YAOMBA SERIKALI KUWATAZAMA WASTAFU WANAOLIPWABLAKI MOJA
Posted on: May 2nd, 2024Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoa wa Kigoma katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, (Mei mosi) wameiomba serikali kuwatazama wastaafu wa zamani ambao bado wanalipwa shilingi laki moja kwa mwezi.
Akizungumza kupitia hotuba iliyoandaliwa na chama hicho, katibu wa TUCTA, Jumanne Magulu ametaja kuwa wastaafu hao wanaishi maisha magumu kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda bei kwa bidhaa.
“Tunaomba serikali iwatazame kwa upya wastaafu hao, iwakumbuke na kuwaongezea kiwango cha fedha ili waweze kujikimu na kukidhi mahitaji yao, laki moja ni pesa kidogo ambayo kwa maisha ya sasa haiwezi kuwasaidia kwa muda mrefu na kuwafanya waishi maisha magumu” amesema Magulu.
Katika hotuba ya chama hicho wameziomba pia taasisi za kifedha kupunguza kiwango cha riba ya mikopo ambapo wamesema kiwango hicho hawawezi kumudu kukilipa.
Sambamba na hilo wameiomba mifuko ya hifadhi za jamii kufuatilia michango ya wanachama katika taasisi husika ili kuepusha changamoto ambazo huwa zinatokea kati ya mwajiri na mwajiriwa hasa katika kipindi cha kufuatilia mafao ambayo yalikuwa hayafikishwi katika mfuko.
Akizungumza Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewaasa wafanyakazi wote kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kubadili mienendo ya utendaji kazi, uwe wa juhudi na wenye maarifa ili kuinua uchumi wa nchi.
Amehimiza ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi wote na kuachana na tabia ya ubinafsi ambayo inafanya watu kukosa haki zao huku ikichochea rushwa na utovu wa nidhamu na hivyo kuharibu utendaji kazi kwa maendeleo.
Andengenye amesema, kufuatia suala la ongezeko la mishahara ambayo ndio kauli mbiu ya maadhimisho hayo kuwa serikali inafanyia kazi mapitio ya sheria ambazo zinakandamiza maslahi ya wafanyakazi hivyo wawe wavumilivu mpaka pale serikali utakapokamilisha mapokeo hayo.
Hata hivyo, amewaonya waajiri wanaowanyanyasa na kuwakandakiza waajiriwa, amewataka wafanye kazi kwa kufuata sheria mpya na kutekeleza haki na wajibu wa kazi, na kwamba waajiriwa wasisite kutoa taarifa kwa waajiri wa namna hiyo ili waadhibiwe sawasawa na kanuni na sheria za nchi