WANANCHI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KIGOMA KUJENGA VYOO NA KUZINGATIA USAFI
Posted on: October 7th, 2024Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt. Rashid Chuachua amewataka wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma kujenga vyoo katika kaya zao ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa Kipindupindu na magonjwa mengine yanayosababishwa na uchafu.
DC Chuachua ametoa kauli hiyo leo tarehe 7 Oktoba,2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mahembe wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa kata hiyo.
"Ugonjwa wa kipindupindu unasababishwa na kula kinyesi kibichi, nataka wananchi wote wawe na vyoo na waache tabia ya kujisaidia na kujisafisha pembezoni mwa mto kwakuwa inasababisha vimelea vya kipindupindu kusambaa kwa urahisi, mwananchi ambaye hana choo atatozwa faini ya shilingi elfu 50,000/= na lazima achimbe choo bora chenye mfuniko na kiwe kisafi" Amesisitiza Dkt. Chuachua
Mhe.Dkt.Chuachua amesema Serikali imejidhatiti kulinda afya ya jamii kwa kuendelea kutoa elimu na huduma bora za afya ili wananchi waendelee kutekeleza majukumu yao ya kujipatia maendeleo wakiwa na afya njema.
Aidha Dkt.Chuachua ameongeza kuwa Serikali haiko tayari kuona watu wanafanya biashara hasa wa chakula katika maeneo yasiyo salama,kwa lengo la kuhakikisha Wananchi hawapati maambukizi ya magonjwa yatokanayo na uchafu ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu.
Pamoja na hayo Mhe.Dkt.Chuachua ametatua kero mbalimbali za migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali,changamoto za ukosefu wa huduma za maji na umeme lakini pia changamoto za vyama vya msingi vya Ushirika(AMCOS) na mfuko wa Maendeleo ya jamii(TASAF).
Dkt.Chuachua ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Wananchi wa Kata hiyo na maeneo mengine kujitokeza katika zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Orodha ya Wapiga Kura wa Serikali za Mitaa na kushiriki Uchaguzi ifikapo 27 Novemba, 2024.